Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatma ya watu wa asili yaangaziwa kwenye Umoja wa Mataifa

UN Photos/Rick Bajornas
Watu wa asili nchini Ethiopia @

Hatma ya watu wa asili yaangaziwa kwenye Umoja wa Mataifa

Watu wa asili wanakadiriwa kufikia idadi ya milioni 370, sawa na asilimia 5 ya watu waliopo duniani, lakini pia sawa na asilimia 15 ya watu maskini zaidi duniani.

Ili kujadili tatizo hilo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeamua kuitisha kongamano kubwa mwezi Septemba, mwaka huu, ili kubadilishana mitazamo na mifano ya kuiga katika kutunza haki za watu wa asili.

Maandalizi ya kongamano hilo yanafanyika wiki hii, mjini New York, kwa kujaribu kumulika changamoto zinazokumba jamii hizi na kufikisha matarajio yao katika ajenda ya maendelo endelevu baada ya 2015, zikiwemo haki ya kujitawala na kumiliki ardhi, upatikanaji wa haki ya sheria, na utunzaji wa mila na lugha za asili.

Balozi Andrej Logar, mwakilishi wa kudumu wa Slovenia, amesema cha msingi ni kuhakikisha serikali na watu wa asili zishirikiane kwa kuheshimiana, huku Bwana Rodion Sulyandziga, Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Watu wa Asili akisisitiza umuhimu wa kutekeleza yaliyoandikwa kwenye Azimio la Haki za Watu wa Asili.