Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 50 ya G77 na China; Ban asema kuishi wote vizuri inawezekana!

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-Moon akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya kundi la G77 na China huko Santa Cruz, Bolivia. (Picha:UN/Evan Schneider )

Miaka 50 ya G77 na China; Ban asema kuishi wote vizuri inawezekana!

Akiwa ziarani Amerika ya Kusini, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amehotubia mkutano wa viongozi wa kundi la nchi 77, ama G77 na China, unaofanyika Santa Cruz, leo siku ya tarehe 14, Juni.

Ametambua mchango mkubwa wa kundi hilo katika mazungumzo yanayoendelea ndani ya Umoja wa Mataifa, hasa kuhusu maendeleo endelevu na mabadiliko ya tabianchi, akisema G77 imesaidia kuipaza sauti ya nchi zinazoendelea katika jukwaa la kimataifa.

Ameongeza, maendeleo ya nchi zinazoendelea yatafaidika dunia nzima.  Amewakumbusha nchi wanachama kuhusu changamoto zilizopo mbele yao, ikiwemo kuandaa ajenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015, na kufikisha makubaliano kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

Amesema hizo ni fursa ya kuondoa tofauti baina ya nchi za kusini na za kaskazini, na amewaomba nchi za kusini ambazo ni nchi zinazoendelea kuchangia katika shughuli hizo kwa kuonyesha mifano yao na maoni yao mapya.

Halikadhalika, ameeleza kuwa ajenda ya baada ya 2015 inapaswa kuangalia matatizo yote yanayokumba nchi hizo, na kuamua mwelekeo utakaofaa kwa dunia nzima. Ameongeza, cha msingi ni kutokomeza umaskini kwa wote na kuheshimu mazingira mtu anapoishi ili, kwa ujumla, kupata njia ya kuishi vizuri huku akifurahi kuona kwamba swala la “kuishi vizuri” limekuwa maudhui ya mkutano huo.

Hatimaye amesihi nchi zinazoendelea kuimarisha ushirikiano wa kusini kwa kusini ili kuongeza nguvu zao za uwekezaji pesa katika uchumi yao, na pia kwa upande wa utalaam na takwimu.

Amemaliza kwa kumkariri mwandishi hayati Gabriel García Márquez ambaye alipewa tuzo la Nobel la Fasihi mwaka 1982, akisema: bado hatujachelewa tukitaka kujenga dunia ambapo hakuna mmoja atakayeweza kuamua kuua wenzake, ambapo upendo utakuwa wa ukweli, na ambapo kuishi na furaha kutawezekana.