Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban awasili Bolivia, kuzungumza kwenye mkutano wa G77 na China

UN Photo/Evan Schneider
Katibu Mkuu Ban Ki-Moon na mwenyeji wake Rais Evo Morales wa Bolivia baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa kimataifa wa Viru Viru huko mjini Santa Curis De la Sierra. Picha@

Ban awasili Bolivia, kuzungumza kwenye mkutano wa G77 na China

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon yuko nchini Bolivia ambako kesho atashiriki maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa kundi la nchi 77, G-77 na China.

Mara baada ya kuwasili Ban alilakiwa na Rais Evo Morales wa Bolivia ambapo Katibu Mkuu alielezea kile alichoshuhudia akiwa angani ikiwemo jitihada za serikali ya nchi hizo za kufikishia wananchi wake wote mahitaji muhimu bila kujali umbali wa maeneo hayo.

Amesema Umoja wa Mataifa unataka kusaidia serikali ili huduma hizo kama vile za afya zipatikane kwa wananchi wote. Ban amesema wanataka kutokomeza umaskini na watu wawe na maisha endelevu sambamba na sayari dunia na hivyo kila nchi iwe ndogo au kubwa ina jukumu la kutekeleza.

Katibu Mkuu amesema amefurahi kukutana na Rais Morales ili aweze kutaarifu wawakilishi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mjini New York kuwa maendeleo endelevu yanawezekana kwenye kona zote za dunia.