Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya, Tanzania na Uganda zaongoza katika uhalifu wa ujangili wa tembo: CITES

Mustakhbali wa tembo hawa uko mashakani kutokana na ujangili unaolenga meno yao. (Picha@Totuvi ya CITES)

Kenya, Tanzania na Uganda zaongoza katika uhalifu wa ujangili wa tembo: CITES

Zaidi ya tembo 20,000 waliuawa kote barani Afrika katika mwaka 2013, kulingana na ripoti mpya iliyotolewa na Sekritariati ya Mkataba kuhusu Biashara ya Kimataifa katika Viumbe vilivyo Hatarini Kuangamizwa, CITES, hukuKenya,UgandanaTanzaniazikiongoza kwa uhalifu huo. Taarifa kamili na John Ronoh

Taarifa ya John Ronoh

Kulingana na ripoti ya CITES, viwango vya ujangili wa tembo barani Afrika bado ni vya kutisha, ingawa havipandi tena kwa kasikamailivyokuwa kati ya mwaka 2000 na 2011.

Ripoti imesema viwango hivyo vya ujangili vimeendelea kuzidi viwango vya kuongezeka kwa idadi ya tembo, na hivyo kupunguza idadi ya tembo barani Afrika.

Ripoti hiyo inaonyesha pia kuwa, kwa mara ya kwanza, Afrika iliipiku bara Asia kwa idadi ya pembe za tembo zilizokamatwa, kwani zaidi ya kilo 500 za pembe za tembo zilinaswa mnamo mwaka 2013, kabla hazijaondolewa Afrika, hukuKenya,TanzanianaUgandapekee zikichangia asilimia 80 ya pembe hizo zilizokamatwa.

Katibu Mkuu wa CITES, John E Scanlon, amesema hali hii inaashiria kuwepo uhalifu wa kimataifa wa kupangwa katika biashara hii haramu.

 “Tembo wa Afrika wanaendelea kukabiliwa na hatari ya kuangamizwa kutokana na viwango vya juu vya ujangili kwa ajili ya pembe zao, na kuuawa kwa zaidi ya tembo 20,000 mwaka uliopita, kunaonyesha hali bado ni mbaya mno.”