Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban, Baraza la usalama walaani shambulio dhidi ya MINUSMA huko Mali

Mlinda amani wa MINUSMA akiwa katika moja ya lindo nchini Mali. Picha@ Photo MINUSMA/Marco Dormino)

Ban, Baraza la usalama walaani shambulio dhidi ya MINUSMA huko Mali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amelaani vikali shambulio la bomu kwenye kambi ya ujumbe wa Umoja huo nchini Mali , MINUSMA lililosababisha vifo vya walinda amani wanne kutoka Chad na wengine kujeruhiwa ikiwemo askari wa Mali.

Ban amekaririwa na msemaji wake akieleza masikitiko yake kwa tukio hilo huko Aguelhok akituma rambirambi kwa familiai za wafiwa na serikali za Chad na Mali huku akiwatakia ahueni ya haraka majeruhi.

Hata hivyo amesema shambulio hilo halitakwamisha azma ya Umoja wa Mataifa ya kusaidia jitihada za wananchi wa Mali za kufikia amani na utulivu wa kudumu.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa pande zote nchini Mali kutokatishwa tamaa na wavunjifu wa amani ambao amesema kupitia vitendo vyao vya kihalifu wanasaka kuzuia kuwepo kwa ujenzi wa amani endelevu nchini Mali.

Nalo baraza la usalama katika taarifa yake limeshutumu shambulio hilo likisema kuwa halikubaliki na kwamba halitazuia azma yake ya kuhakikisha Mali inapata amani ya kudumu.