Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suala la ukatili wa kingono katika vita lavaliwa njuga London

Zainab Bangura akihotubia kongamano la kimataifa kuhusu kutokomeza ukatili wa kingono katika vita @UNFPA

Suala la ukatili wa kingono katika vita lavaliwa njuga London

Kongamano la kimataifa kuhusu kutokomeza ukatili wa kingono katika vita, limeingia siku yake ya pili mjini London, Uingereza, kwa hotuba kutoka kwa wataalam wa suala hilo. Mmoja aliyezungumza ni Zainab Hawa Bangura, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kingono katika vita.

“Tupo hapa leo kuandika aya ya mwisho katika historia ya ubakaji katika nyakati za vita, na kufunga kitabu cha uanadamu kuunyamazia unyama huu.”

Bi Bangura amesema kuhudhuriwa kwa kongamano hilo kwa wingi ni ishara ya matumaini kwa manusura na jamii zilizoathiriwa kuwa ubakaji si unyanyapaa wa kuvumiliwa kimya kimya.

“Ubakaji katika maeneo ya vita ni moja ya masuala ya kipaumbele zaidi ya usalama wa kimataifa katika nyakati zetu. Ukitekeleza, au kuamrisha au kupuuza ukatili wa kingo katika migogoro, tutakuandama kwa njia na uwezo wote tulio nao. Hakutakuwa na pa kujificha. Punde, tutakupata.”

Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na serikali ya Uingereza, limewaleta pamoja watu mashuhuri kama vile nyota wa filamu, Angelina Jolie, na wanaharakati wanaopinga ukatili wa kingono.