Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ILO yapitisha mkataba mpya wa kukabiliana na ajira za lazima

UN Photos
Guy Rider, mkurugenzi mkuu wa ILO @

ILO yapitisha mkataba mpya wa kukabiliana na ajira za lazima

Shirika la Kazi Duniani, ILO, limepitisha mkataba wa kisheria ulioundwa kwa minajili ya kuimarisha juhudi za kimataifa za kuzuia na kutokomeza ajira za kulazimishwa pamoja na utumwa wa kisasa. Taarifa kamili na George Njogopa

(Taarifa ya George)

Mkataba huo umepitishwa kwa kura 437 za wawakilishi wa serikali, waajiri na waajiriwa ambao wanahudhuria kongamano la kimataifa la kazi mjini Geneva, pamoja na kutolewa pendekezo la jinsi ya kuutekeleza.

Mkataba huo unabadilisha ule ambao umekuwepo tangu mwaka 1930 na kuufanya uwe wa kisasa, ili kukabiliana na vitendo kama usafirishaji haramu wa watu. Pia unajumuisha masuala ya ulinzi na ulipaji fidia kwa waathiriwa.

Akizungumza baada ya kuupitisha mkataba huo, Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Guy Ryder amesema mkataba huo na pendekezo la utekelezaji wake ni hatua ya kwanza katika kupiga vita ajira za lazima, na pia ari ya kuutokomeza utumwa wa nyakati za sasa.