Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kisa cha polio charipotiwa Somalia

watoto wakipewa chanjo mwaka 2013 @UNICEF Somalia

Kisa cha polio charipotiwa Somalia

Kisa cha kwanza cha polio kwa mwaka huu nchini Somalia kimethibitishwa tarehe 4, mwezi Juni, kwenye maeneo ya kaskazini mwa kati ya nchi, kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Kuratibu Missada ya Kibinadamu, OCHA.

Akizungumza leo mbele ya waandishi wa habari, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amesema kwamba kuibuka tena kwa ugonjwa huo wa polio mwaka huu kunakwamisha mafanikio yaliopatikana mwaka jana baada ya kampeni kubwa ya chanjo.

Dujarric ameongeza kwamba timu ya wataalam wa polio inajiandaa kutoka Nairobi kutathmini hali ilivyo sasa hivi.

Mwaka 2013, kulitokea mkurupuko wa polio nchini Somalia, kwa mara ya kwanza baada ya 2007, wakati nchi hiyo ilikuwa imefanikiwa kutokomeza kabisa ugonjwa huo nchini. Mashirika ya kimataifa yakiwemo lile la kuhudumia watoto, UNICEF, yalifanikiwa kuwapatia watoto zaidi ya milioni 4 chanjo za polio na hivyo kusitisha mkurupuko wa ugonjwa huo Somalia. Kampeni hiyo ilitajwa pia kama mfano wa kufikisha huduma za afya katika maeneo yaliyo mbali na barabara.