Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makabila kinzani huku Darfur Kaskazini yakutatanishwa:UNAMID

Baadhi ya viongozi hao wa makabila kinzani huko Darfur Kaskazini kwenye mkutano huo. @UNAMID

Makabila kinzani huku Darfur Kaskazini yakutatanishwa:UNAMID

Huko Darfur Kaskazini nchini Sudan hii leo kumeanza mkutano wa siku mbili ukijumuisha wawakilishi zaidi ya 250 wa makabila ya Beni Hussein na Abbala , mkutano unaofanyika kwenye eneo la Kabkabiya,El Fasher chini ya uratibu wa ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika, UNAMID.

Pande mbili hizo kwa siku za hivi karibuni zimekuwa na mivutano iliyosababisha mapigano, kufungwa kwa barabara na hivyo kushindwa kusafirishwa kwa mahitaji muhimu kama vile vyakula, dawa na mafuta kwende eneo la El Sereif .

Mkuu wa UNAMID kitengo cha kaskazini Mohamed El-Amine Souef akizungumza kwenye mkutano huo uliojumuisha pia maafisa wa serikali amesisitiza azma ya ujumbe huo kuendelea na mamlaka yake ya kulinda raia, na kusaidia jitihada za maridhiano zinazotekelezwa na wakazi wa eneo hilo bila kusahau usaidizi wa kibinadamu.

Hata hivyo ametaka pande zote kuunga mkono juhudi za sasa za maridhiano akisema kuwa bila amani hakuna maendeleo na bila amani Darfur hakuwezi kuwepo na utulivu Sudan.