Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya mazingira duniani, nchi za visiwa vidogo zinazoendelea zamulikwa

Siku ya mazingira duniani, nchi za visiwa vidogo zinazoendelea zamulikwa

Ikiwa leo ni siku ya mazingira duniani, nchi za visiwa vidogo zinazoendelea zimetajwa kuwa ndio zinazohaha zaidi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabiachi duniani.

Katika ujumbe wake wa siku hii inayomulika nchi hizo, Katibu Mkuu Ban Ki-Moon ametaka kila mtu kupaza sauti kulinda mazingira badala ya kuongeze kiwango cha maji ya bahari.

Ban amesema hayo wakati shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP likitaja sababu za nchi hizo kuwa hatarini zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Mkuu wa kitengo cha UNDP kinachohusika na mazingira na nishati Nik sekhran ameiambia Radio ya Umoja wa Mataifa kuwa sababu kuu ya maeneo hayo kuwa hatarini zaidi ni kutokana na kuwa ukanda wa chini zaidi.

(Sauti ya Keran)

“Na hilo ndilo linafanya ziwe hatarini zaidi kwa mabadiliko ya tabianchi. Kiwango cha maji ya bahari kikiongezeka, mawimbi yanaongezeka. Visiwa hivyo pia vinategemea zaidi eneo dogo la ardhi kwa ajili ya kilimo na kadhalika. Iwapo mazingira yanamomonyoka, hii inaharibu kabisa uchumi wao.”

Tayari Katibu Mkuu ameitisha mkutano wa viongozi mwezi Septemba mwaka huu mjini New York akitaka serikali kuja na hatua za kijasiri za kulinda mazingira ikiwemo kuhakikisha makubaliano mapya ya mabadiliko ya tabianchi yanafikiwa mwakani.