Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hifadhi ya jamii bado ni tatizo kwa zaidi ya asilimia 70 ya wakazi duniani:ILO

Nakala za ripoti ya ILO kuhusu haliya hifadhi ya jamii duniani.(Picha@Unifeed)

Hifadhi ya jamii bado ni tatizo kwa zaidi ya asilimia 70 ya wakazi duniani:ILO

Shirika la kazi duniani ILO limetoa ripoti yake inayosema kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wakazi ulimwenguni hawapati hifadhi ya jamii.

Ripoti ya ILO iitwayo Hifadhi ya jamii duniani, kujenga ukwamuaji wa kiuchumi, maendeleo jumuishi na haki ya kijamii inasema wanaopata haki hiyo kwa uhakika ni asilimia 27 tu licha ya makubaliano ya kimataifa ya mwaka 1948 yaliyoeleza kuwa hifadhi ya jamii na huduma za afya kwa watoto, watu wanaokabiliwa na ukosefu wa ajira, ajali kazini au wazee ni haki ya msingi kwa wote.

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa ILO Sandara Polaski anasema katika zama hizi za kutotabirika kwa hali ya uchumi, kiwango kidogo cha ukuaji uchumi na kuongezeka kwa tofauti za kipato hifadhi ya jamii inakuwa ni jambo linalochagizwa zaidi.

(Sauti ya Sandra)

"Jambo muhimu linalotakiwa sasa ni kuhakikisha ajenda ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015 inapatia kipaumbele suala la hifadhi ya jamii kwani uchumi unaposuasua marekebisho ya uchumi mara nyingi hukumba sekta hiyo na siyo tu katika nchi tajiri hata zile zinazoendelea. Na katika kuimarisha uchumi serikali 122 zimebana matumizi ambapo 82 ziko nchi zinazoendelea ambapo hatua zinahusisha pamoja na kupunguza wigo wa mafao ya pensheni, bima za afya na ustawi wa jamii."