Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban amtembelea Meya wa New York

Katibu Mkuu Ban Ki-moon: Picha ya UM

Ban amtembelea Meya wa New York

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amemtembelea Meya mpya wa mji wa New York, Bill de Blasio kwenye ofisi yake, ya City Hall, ambako wamejadili kuhusu mabadiliko ya tabianchi na masuala mengine.

Bwana Ban amesema miji mikubwa kama New York inakabiliwa na tishio la moja kwa moja kutokana na mabadiliko ya tabianchi, ingawa pia inatoa fursa za ubunifu.

Ban amesema kuwa yeye na Meya de Blasio walijadiliana kuhusu kutahadhari kwa majanga kama kimbunga Sandy na kupunguza madhara ya majanga ya siku zijazo.

Ban amemshukuru Meya huyo pia kwa ushirikiano wake katika kukarabati makao makuu ya Umoja wa Mataifa, akisema kuwa Umoja wa Mataifa hupewa msukumo mkubwa kutoka kwa makao yake mjini New York.

Katibu Mkuu amesema anatarajia kushirikiana na Meya de Blasio na uongozi wake, akiongeza kuwa huu ni wakati wa mtihani na mabadiliko kote duniani.

Bwana Ban amesema kuwa amemwalika Meya huyo kuhudhuria mkutano mkuu wa mabadiliko ya tabianchi mnamo Septemba 23 kwa sababu ahadi yake kuufanya mji wa New York uwe unaojali mazigira zaidi.