Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akutana na Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, wajadili DRC na Burundi

UN Photos/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akiwa na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania. @

Ban akutana na Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete, wajadili DRC na Burundi

Akihudhuria kongamano kuhusu afya ya wakina mama na watoto, Toronto, nchini Canada, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekutana na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania.

Ban amempongeza Kikwete kwa mwongozo wake katika maswala ya maendeleo endelevu, akiwa Mwenyekiti wa Kamisheni kuhusu Elimu na Uwajibikaji kwa Afya ya Watoto na Wakina Mama, na pia katika Kamati ya Viongozi wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi.

Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo kumwalikwa Rais Kikwete kuhudhuria kongamano la Tabia Nchi litakalofanyika Septemba, tarehe 23, mjini New York.

Wawili hao pia wamekubaliana kuhusu umuhimu wa kufikia maelewano ya kudumu kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.

Katibu Mkuu amesisitiza pia umuhimu wa kuchukua hatua ili kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia na kushughulikia ajenda ya maendeleo endelevu baada ya mwaka 2015.

Wamezungumzia hali ya usalama ya Ukanda wa Maziwa Makuu. Katibu Mkuu ameishukuru Tanzania kwa mchango wake katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, MONUSCO, ikiwemo katika kikosi maalum cha kujibu mashambulizi.  Wamekubali kwamba ni lazima kuondoa vikundi vya waasi vinavyotishia DRC, hasa FDLR. Halikadhalika, walijadili kuhusu Burundi.