Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lazima tujiandae kwa ukuaji wa miji: Rais Kagame

Lazima tujiandae kwa ukuaji wa miji: Rais Kagame

Wakati mkutano ulioandaliwa na Baraza la Uchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa, ECOSOC, unaendelea mjini New York, Marekani, kwa kuangalia jinsi ujenzi wa miji na ongezeko la wakazi wa miji vinachangia katika maendeleo endelevu, raisi wa Rwanda Paul Kagame amezungumzia mfano wa mji wa Kigali, akisema miji inaendelea kukua, na hakuna jinsi ya kuzuia mwelekeo huo.

Amesema kasi ya ukuaji huo itaendelea kuongezeka, hasa kwa bara la Afrika, ambako mpaka sasa hivi idadi ya watu wanaoishi mjini ni ndogo kuliko sehemu nyingine duniani.

Lakini kuishi mjini, kwa mujibu wa Bwana Kagame, ni fursa, kwani watu wakihamia mjini wanabadilika, wanajifunza teknolojia na ujuuzi mpya, na kwa ujumla, wanaweza kujiendeleza zaidi kiuchumi.

Ili ukuaji wa miji ufaidishe raia wote, wawe mjini au shambani, ni lazima serikali na watu wajitahadhari, waandae mipango miji na waitekeleze kwa njia endelevu.

Rais wa Rwanda amesema, mji wa Kigali unakabiliana na changamoto hizo hizo, na majukumu ya serikali yamekuwa pamoja na kuboresha na kuzuia makazi holela, kujenga miundu mbinu imara, kulinda maeneo ya rasilimali na pori yaliyoko mjini, na kuwezesha sekta binafsi kupatia ajira kwa vijana.

Amesisitiza juhudi za serikali katika kuhakikisha kuwepo kwa hati miliki ya ardhi kila sehemu na takwimu sahihi ili kuimarisha soko hilo.

Hatimaye, katika mahojiano maalum na ECOSOC, amesema kwamba mafanikio hayo yamesababishwa pia na ushirikishi kamilifu wa jamii katika ngazi zote za maamuzi ya mipango miji, kupitia mfumo wa serikali za mitaa.