Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

“Ubinadamu unahujumiwa Syria”: Ripoti ya UNRWA na UNDP

@UNRWA

“Ubinadamu unahujumiwa Syria”: Ripoti ya UNRWA na UNDP

Ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwasaidia Wakimbizi wa Palestina, UNRWA, Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP, na Kituo cha Utafiti wa Kisera nchini Syria, imesema kuwa mzozo wa Syria umeweka mazingira ya ukatili unaokiuka haki za binadamu, uhuru wa raia na utawala wa sheria, huku watu wenye nafasi za juu kisiasa na kiuchumi wakitumia mitanadao yao ya kitaifa na kimataifa kufanya ulanguzi wa silaha, bidhaa na usafirishaji haramu wa watu.

Ripoti hiyo imesema watu hao pia wanaitumia hiyo mitandao kufanya wizi na utekaji nyara, na hata ufujaji wa misaada ya kibinadamu, ikihitimisha kuwa mazingira haya pia yanawapa watu hawa hamu ya kutaka kuuendeleza mzozo huo.

Mkurugenzi wa huduma za fedha katika UNRWA, Alex Pollock amesema kuwa Syria imeghubikwa na ukosefu wa ajira, akiongeza kuwa tangu mzozo uanze, watu milioni 11 wamepoteza vitega riziki vyao, huku watu milioni 2.7 wakipoteza ajira.

Kulingana na ripoti hiyo iitwayo, “Kubadiri Ubinadamu”, ambayo inaangazia miezi sita ya mwisho ya mwaka 2013, deni la kitaifa liliendelea kuongezeka, wakati serikali ilipoagiza mafuta na bidhaa za kimsingi ili kukabiliana na uhaba kwenye soko la kitaifa. Msemaji wa UNRWA, Chris Gunness amesema ni vigumu kupima athari za kijamii na madhara kwa watu binafsi.