Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akaribisha kupitishwa azimio la majukumu mapya ya UNMISS

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-Moon. (Picha:UN/Maktaba)

Ban akaribisha kupitishwa azimio la majukumu mapya ya UNMISS

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amekaribisha kupitishwa kwa azimio namba 2155 (2014) kuhusu Sudan Kusini, ambalo limefanyia marekebisho majukumu ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS. Azimio hilo lililopitishwa jioni mnamo Jumanne ya tarehe 27 Mei, linayapanua majukumu ya UNMISS ili ijikite zaidi katika ulinzi wa raia, kufuatilia hali ya haki za binadamu, na kusaidia katika ufikishaji wa misaada ya kibinadamu kwa walengwa.

Kwa azimio hilo pia, idadi ya askari walinda amani wa UNMISS imeongezwa hadi kufikia 12,500, kulingana na ombi la Katibu Mkuu katika ripoti yake ya hivi karibuni zaidi kuhusu Sudan Kusini.

Bwana Ban pia amekaribisha kujumuishwa kwa kundi la kuchukua hatua la IGAD katika UNMISS, ili lisaidie katika ulinzi wa raia na katika mfumo wa kufuatilia na kuhakiki hali ya mambo. Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa majukumu hayo mapya katika kurejesha amani na usalama Sudan Kusini, na kurejelea ujumbe wake kuwa kila juhudi zifanywe ili wanaochangia askari walinda amani na wahudumu wengine kwa UNMISS wafanye hivyo haraka iwezekanavyo.