Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Makubaliano ya kusitisha mapigano Kidal yawezesha usambazaji wa misaada:OCHA

Waathiriwa wa mapigano -Mali(Picha@MINUSMA)

Makubaliano ya kusitisha mapigano Kidal yawezesha usambazaji wa misaada:OCHA

Nchini Mali watoa huduma za misaada wameanza tena operesheni zao baada ya mashirika ya Umoja wa Mataifa kufikisha misaada kama vile maji, vyakula na vifaa tiba. Usambazaji wa vifaa hivyo umewezekana kutokana na makubaliano ya tarehe 23 mwezi huu ya kusitisha mapigano kati ya mamlaka za Mali na vikundi vya waasi.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya usaidizi wa kibinadamu, OCHA imesema takribani watu Elfu nne walikimbia mji wa Kidal kaskazini mwa Mali baada ya mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi siku kumi zilizopita.

Kwa sasa wakimbizi wa ndani wapatao Elfu Moja wamepata hifadhi kwa wenyeji wa mji wa Gao. Jens Learke anasema kuwa Umoja wa Mataifa unafanya kila iwezelo ili kusaidia wakazi hao.

"Tangu Aprili, hali ya usalama iliyokuwa ikizorota kwa kasi ilikwamisha mashirika ya Umoja wa Mataifa kuwepo maeneo hayo, lakini mashirika ya kiraia yaliendelea na kazi zao kupitia wadau wao eneo hilo. Wadau hao huko Kidal wametoa misaada tangu kuanza kwa ghasia, hususan misaada kwa majeruhi na kufuatilia waliokimbia makazi.”

OCHA inasema baadhi ya wakimbizi wa ndani wameweza kurejea nyumbani kwao huko Kidal huku watoa huduma za misaada wakijikita kutathmini mahitayo yao.