Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji ya mlinda amani Darfur, Ban atuma rambirambi, azungumzia pia Libya

Mauaji ya mlinda amani Darfur, Ban atuma rambirambi, azungumzia pia Libya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amelaani mauaji  ya mlinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Rwanda aliyeuawa huko Kabkabiya, Darfur Kaskazini nchini Sudan Jumamosi asubuhi.

Mlinda amani  huyo aliuawa na wengine watatu walijeruhiwa baada ya jaribio la kusuluhisha mzozo baina ya makundi mawili yaliyojihami, kushindikana. Makundi hayo  yasadikiwa ni lile la waarabu na kabila la Fur.

Majeruhi hivi sasa wanapatiwa matibabu kwenye kituo cha ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika Daruf, UNAMID ambapo Ban ametuma rambirambi kwa familia ya mlinda amani huyo kutoka Rwanda pamoja na serikali huku akiwatakia majeruhi wapate nafuu mapema.

Katika hatua nyingine, taarifa ya msemaji wa umoja wa Mataifa imemkariri Bwana Ban akielezea wasiwasi wake juu ya kile kinachoendelea Libya hususan ongezeko la uimarishaji wa vikosi vya kijeshi kwenye mji mkuu Tripoli.

Katibu Mkuu amesema mizozano ya kijeshi inahatarisha harakati za wananchi wa Libya za kujitoa kwa dhati kwa ajilia ya uhuru na utu wao hususan kwenye mchakato wa sasa wa mpito kisiasa.

Bwana Ban ametaka pande zote na viongozi wa kijeshi kuzingatia wajibu wao wa kimaadili na kisheria ili kulinda raia.

Halikadhalika ametaka pande hizo kujizuia kufanya vitendo vyovyote vinavyoweza kudidimiza kipindi cha sasa cha mpito na wakati huo huo warejee katika meza ya mazungumzo kwani Umoja wa Mataifa kupitia mwakilishi wake Libya uko tayari kuwezesha mchakato huo kwa maslahi ya taifa hilo.