Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UN-Women na mjumbe kutoka AU wawasili CAR:

Wengi wanaothirika na janga linaloendelea CAR ni wanawake na watoto. Kama wanavyoonekana hapa wakimbizi wa ndani wakichota maji. (Picha ya © UNHCR/A.Greco)

Mkuu wa UN-Women na mjumbe kutoka AU wawasili CAR:

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na wanawake, UN-Women, Phumzile Mlambo-Ngcuka amewasili Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, kwa ziara ya siku tatu ya kuangalia hali ya wanawake na wasichana wakati huu wanapokukumbwa na machungu ya mapigayo yanayoendelea nchini mwao.

Mara baada ya kutua Bangui Bi. Mlambo-Ngcuka amesema..

"Wanawake na wasichana ni kipaumbele chetu tukiangazia ukatili dhidi yao na suala la elimu na mahitaji ya kibinadamu ya wananchi wote.”

Mkurugenzi mtendaji huyo wa UN-Women ameambatana na Bineta Diop mjumbe maalum wa Muungano wa Afrika kwa masuala ya wanawake, amani na usalama ambaye ameweka bayana kuwa..

(Sauti ya Diop)

"Tuko hapa kuonyesha mshikamano na wanawake wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Tuko hapa pia kuunga mkono juhudi za serikali ya CAR. Tuko hapa pia kushuhudia wanawake ambao ni waathirika pamoja na watoto. Kwa sababu naamini kile tunapaswa kufanya ni kuwapatia matumaini. Pia kuwasaidia kwa ajili ya maridhiano na ujenzi wa nchi yao. Sasa iwe ni Afrika, iwe ni Umoja wa Mataifa, lakini kwa ujumla ni wanawake wa Afrika  tuko hapa kwa mshikamano ili kuwaambia kuwa tuko pamoja kuwasaidia.Tunataka kuiambia dunia angalia kile tulichoshuhudia nchini humo.” 

Wakati wa ziara hiyo, viongozi hao kutoka Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika watakutana na viongozi waandamizi wa serikali ya mpito ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, pamoja na wawakilishi wa vikundi vya kiraia, wanawake, wakimbizi wa ndani na viongozi wa kidini.