Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kura ya kuipeleka kesi ya Syria kwa ICC yapingwa na Urusi

Naibu wa katibu Mkuu Jan Eliason Wakati wa kikao cha Baraza la Usalama (Picha ya UM/Evan Schneider)

Kura ya kuipeleka kesi ya Syria kwa ICC yapingwa na Urusi

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limeshindwa kupitisha azimio la kuipeleka kesi ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na uhalifu wa kivita nchini Syria kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC.

Nchi kumi na tatu wanachama wa Baraza hilo zimeunga mkono mswada wa azimio hilo, lakini kwa sababu ulipingwa na Urusi, mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama, huku Uchina ikionyesha kutoegemea upande wowote, mswada huo haukupitishwa.

Mapema kabla ya kura hiyo, ujumbe wa Katibu Mkuu kwa Baraza la Usalama ulisisitiza kuwa uwajibikaji kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaweza kuzuia ukatili zaidi nchini Syria. Ujumbe wa Bwana Ban umesomwa na Naibu wake Jan Eliasson kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

(JAN ELIASSON)

“Tangu kuibuka kwa mzozo Syria, nimerejea mara kwa mara umuhimu wa uwajibikaji kwa wahusika wa uhalifu huu mkubwa wa ukiukwaji wa haki za binadamu, uhalifu dhidi ya binadamu na hata wa kivita. Mashambulio ya  hivi karibuni dhidi ya misafara ya misaada ya kibinadamu na watendaji, ambayo yanaweza kuwa ni uhalifu wa kivita, yanaongeza udharura wa kuchukua hatua sasa za uwajibikaji Syria.”