Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuzorora kwa usalama Mali kwamtia shaka Ban

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephen Dujarric.(Picha UM/Maktaba)

Kuzorora kwa usalama Mali kwamtia shaka Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema kuendelea kuzorota kwa usalama huko Kidal nchini Mali kunazidi kumtia wasiwasi mkubwa akitaka mapigano yakome mara moja na kufikiwa kwa makubaliano ya kuyasitisha.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephen Dujarric amewaambia waaandihi wa habari kuwa Ban ana wasiwasi zaidi na usalama wa raia na amerejea kuwa usalama wa raia ni wajibu wa kila pande huku akitaka wahusika wawajibishwe kisheria.

(Sauti ya Dujarric)

“Katibu Mkuu amesisitiza wito wa Baraza la Usalama wa kutaka kuanza tena kwa mazungumzo ya amani yaliyo shirikishi na ya dhati baina ya pande zilizotia saini makubaliano ya awali Ouagadougou.”

Hivi karibu Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson alieleza hayo bayana kwa Rais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa na kiongozi kutoka Muungano wa Ulaya ambaye naye pia ameelezea wasiwasi wake juu ya kinachoendelea Mali.