Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pillay alaani uvunjifu wa haki za binadamu Allepo

Kamishna wa Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu Navi Pillay (Picha ya Unifeed)

Pillay alaani uvunjifu wa haki za binadamu Allepo

Kamishna wa Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu Navi Pillay amelaani vikali juu ya kile alichokiita kukithiri kwa vitendo vinavyokwenda kinyume na sheria za kimataifa na uvunjivu wa haki za binadamu katika eneo la Allepo nchini Syria, vitendo ambavyo hufanywa na serikali na makundi ya waasi.

Kamishna huyo amesema kuwa mamia ya raia katika eneo hilo wanishi katika mazingira ya hofu kutokana na kuongezeka kwa matukio ya mashambulizi ambayo yamesababisha pia wengi kuyahama makazi yao na wengine hata kupoteza maisha.

Mashambulizi hayo ambayo baadhi yake ni yale ya angani yameripotiwa kuongezeka katika kipindi cha miezi sita iliyopita na kwamba yamevuruga pia ustawi wa kijamii na kuharibu miundo mbinu.

Kumekuwa na wasiwasi wa kujitokeza kwa athari za kiafya kutokana na sehemu kubwa ya eneo hilo kukosa huduma muhimu ikiwamo maji.

Ripoti zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zimebainisha kuwa vyanzo vya maji kwenye eneo hilo viko katika hali mbaya kutokana na kutokarabatiwa kwa kipindi kifefu.