Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ustawi wa karne ya 21 uko mashakani; Ban awaeleza viongozi wa CICA

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-Moon akiwa na baadhi ya viongozi wa CICA. (Picha:UM/Mark Garten)

Ustawi wa karne ya 21 uko mashakani; Ban awaeleza viongozi wa CICA

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amezungumza katika kikao cha viongozi wa mkutano wa mashauriano ya kujengeana imani huko Asia, CICA na kusema kuwa matumaini ya ustawi katika karne hii ya 21 yanakabiliwa na vitisho kadhaa ambavyo ni lazima vishughulikiwe kwa pamoja. Alice Kariuki na ripoti kamili.

(Ripoti ya Alice)

CICA, jukwaa la nchi wanachama 26 barani Asia linatambua kuwa ushirikiano wa kiuchumi unachagiza amani, utulivu na usalama kwenye ukanda huo, hata hivyo Ban akizungumza wakati wa kikao cha leo huko Shanghai amesema bara la Asia linaibuka likiwa na matumaini na kuwa mfano kwa dunia lakini kuna mambo matano yanayotishia ustawi huo. 

Mosi ni mzozo wa Syria, pili hofu ya nyuklia kwenye rasi ya Korea, tatu mizozano baina ya nchi wanachama wa CICA, nne mabadiliko ya tabianchi na tano ni uhalifu na ugaidi. Hivyo akasema..

“Hebu na tutibu vidonda vitokanavyo na historia na tumalize tofauti zetu kwa njia ya ushirikiano na siyo mizozonano! Kwa kuzingatia maslahi ya pamoja na siyo hatua za upande mmoja! Kama usemi wa kichina unavyotukumbuka kuwa tundu dogo lisipozibwa kwa wakati litakuwa shimo kubwa na itakuwa vigumu zaidi kuziba. Wakati mnajengeana imani baina yenu, mtajenga madaraja yafakayofanya dunia iwe pahala bora zaidi kwa watu wote.”

CICA ilianzishwa mwaka 1992 wakati mkutano wa 47 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa pendekezo la Kazakhstan.