Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mustakhbali wa sekta ya afya, wahudumu, wagonjwa mashakani:WHO

Mkutano wa kikao cha 67 cha baraza kuu la WHO (Picha ya WHO/V. Martin)

Mustakhbali wa sekta ya afya, wahudumu, wagonjwa mashakani:WHO

Huko Geneva, Uswisi katika kikao cha Baraza Kuu la shirika la afya duniani, WHO, kumefanyika mjadala wa kiufundi ukiangazie vile ambavyo sekta ya afya inakumbwa na mashambulizi siyo tu wakati wa amani bali pia wakati wa mizozo na hata wakati wa majanga ya kibinadamu.

Mkurugenzi Mtendaji wa WHO Dkt. Margaret Chan amesema vituo vya afya, magari ya wagonjwa, wahudumu wa afya na hata wagonjwa hushambuliwa mara kadhaa na hilo ni kinyume na sheria za kimataifa za kibinadamu zinazotaka maeneo na makundi hayo kulindwa katika mazingira yoyote. Dkt. Chan akarejelea azimio la baraza kuu la WHO la mwaka 2002..

(Sauti ya Dkt. Chan)

Katika siku za karibuni kilio dhidi ya matukio  haya kimepungua! Hisia za janga hili zimenyamazishwa! Na mashambulizi haya yamezidi kuenea! Hii haiweze kuvumiliwa kuwa ni utamaduni mpya. Tunapaswa kuelimisha upya ulimwengu kuhusu hali hii ambayo haikubaliki kabisa. Na wahudumu wa afya wanawajibu wa kutibu majeruhi bila ubaguzi wowote.Nchi zinapaswa kuheshimu wajibu huo.”

 Kikao hicho kimeangazia majanga yanayokumba sekta ya afya na wagonjwa huko Sudan Kusini, Syria, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Colombia na Ufilipino.