Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban akiwa China, akutana na Marais wa Urusi na Pakistan

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-Moon katika mazungumzo yake na Rais Vladmir Putin wa Urusi. (Picha:UM/Mark Garten)

Ban akiwa China, akutana na Marais wa Urusi na Pakistan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliyeko ziarani huko China amekuwa na mazungumzo na viongozi mbali mbali akiwemo Rais Vladmir Putin wa Urusi ambapo wamejadili masuala kadhaa ikiwemo changamoto za amani na usalama duniani hususan hali ilivyo Ukraine na Syria.

Mathalani katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kando mwa mkutano wa mashauriano ya kujengeana imani huko Asia, CICA, Ban na Putin wamekubaliana kuwa mzozo wa Ukraine unaweza kusuluhishwa kisiasa kupitia majadiliano shirikishi.

Ban amesema uchaguzi ujao wa Rais ni fursa ya kusongesha mbele amani na utulivu wa kudumu. Kuhusu Syria wamejadili suluhisho la kisiasa lililochukua muda hadi sasa kupatikana na kusababisha mamilioni ya watu kukimbia makazi yao.

Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, Katibu Mkuu amerejelea umuhimu wa makubaliano ya kimataifa mwakani kuhusu suala hilo na kukumbushia mkutano wa mabadilko ya hali ya hewa utakaofanyika Septemba mwaka huu mjini New York.

Halikadhalika Ban amekuwa na mazungumzo na Rais  Mamnoon Hussain wa Pakistani na kuangazia hali za kibinadamu nchini humo pamoja na uhusiano wake na Afghanistan.

 

Ameshukuru mchango wa Pakistani kwenye ulinzi wa amani unaofanywa na Umoja wa Mataifa kwa kuchangia polisi akisema watendaji hao wanafanya kazi nzuri katika mazingira magumu.