Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IPU yaingia hofu na kinachoendelea Thailand

Nembo ya IPU

IPU yaingia hofu na kinachoendelea Thailand

Tunahofu kubwa na kinachoendelea hivi sasa nchini Thailand, umesema muungano wa mabunge duniani, IPU wakati huu ambapo serikali ya nchi hiyo imepitisha sheria ya kijeshi kwa lengo la kile inachodai kurejesha utulivu.

Rais wa IPU Abdelwahad Radi amesema wanatiwa hofu na mgawanyiko katika siasa za Thailand kwa miaka kadhaa sasa na kwamba mzozo umezidi kuimarika siku za karibuni na kutaka hali hiyo ipatiwe suluhisho la kisiasa.

Amesema kwa mustakhbali wa demokrasia nchini Thailand ni vyema pande zote zinazokinzana kushiriki katika mazungumzo ya kuleta maelewano kwa maslahi ya wananchi wote na hatimaye uchaguzi huru na wa haki ufanyike haraka iwezekanavyo.

IPU imerejelea wito wake kuwa bunge lililochaguliwa na wananchi wote ni msingi wa demokrasia na hivyo ni vyema siyo tu kuandaa uchaguzi haraka bali pia kuhakikisha vyama vyote vya siasa vinaheshimu matokeo ya uchaguzi huo.

IPU imekuwa ikishirikiana na bunge la Thailand katika kutatua mambo kadhaa ikiwemo yale yanayohusu haki za binadamu.

Mathalani ilishauri Thailand kutumia mahakama kutatua masuala ya kisiasa lakini hali imekuwa ngumu katika kutofautisha uhuru wa nguzo tatu za dola ambazo ni serikali, bunge na mahakama.