Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM wachagiza sekta ya biashara kubadili mwelekeo kuhusu majanga

Katibu Mkuu Ban Ki-moon

UM wachagiza sekta ya biashara kubadili mwelekeo kuhusu majanga

Kufuatia taarifa ya Katibu Mkuu Ban Ki-moon kuwa hasara za kiuchumi zimekithiri na kwamba zinaweza tu kupunguzwa kupitia ubia katika sekta ya kibinafsi, Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na kupunguza hatari za majanga, UNISDR, imezindua leo mkakati wa R!SE, ambao utajumuisha udhibiti wa tahadhari za majanga mpiango ya biashara na maamuzi ya uwekezaji.

Mkakati wa R!SE unaleta pamoja wenye umaarufu mkubwa katika biashara, uwekezaji, bima, sekta ya umma, elimu ya biashara na kampuni za kiraia kubuni na kuendeleza viwango vya kimataifa vya uwekezaji unaozingatia tahadhari dhidi ya majanga, kufuatia miaka kumi ya hasara na usumbufu wa kuvunja rekodi katika uchumi.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, amewapongeza viongozi wa kibiashara na UNISDR kwa kuuzindua mkakati huo wa R!SE, akisema kuwa unatoa mwarobaini mpya wa kuepukana na hasara za kiuchumi kutokana na majanga, ambayo hukwamisha kwa kiasi kikubwa ukuaji na maendeleo ya kiuchumi. Naye Mkuu wa UNISDR, Margareta Wahlström, amesema wanaofanya mipango na maamuzi ya uwekezaji wanatakiwa kuzingatia tahadhari za majanga, na kwamba wanadaiwa na wateja na wafanyakazi wao kufanya hivyo.

Ubia huo mpya unajumuisha PricewaterhouseCoopers (PwC), Economist Intelligence Unit (EIU), Chuo cha Kimataifa cha Florida(FIU), Principles for Responsible Investment (PRI), AECOM na Willis.