Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jose Mourinho awa balozi mwema wa WFP

Naibu Mkurugenzi,WFP na mkuu wa operesheni Amir Abdulla na Jose Mourinho (Picha ya WFP)

Jose Mourinho awa balozi mwema wa WFP

Mmoja wa mameneja wa timu za soka mwenye mafanikio zaidi ulimwenguni, Jose Mourinho ameteuliwa na shirika la mpango wa chakula duniani, WFP kuwa balozi mwema wa kutokomeza njaa.

Mourinho ambaye kwa sasa ni meneja wa klabu ya Chelsea ya Uingereza atatumia hadhi yake kueneza ujumbe wa WFP wa kuokoa maisha kwa kutokomeza njaa ulimwenguni kote.

Naibu Mkurugenzi wa WFP ambaye pia mkuu wa operesheni za shirika hilo Amir Abdulla amesema Mourinho amepata karibu mafanikio yote kwenye soka na wanafurahia kuwa sasa anachkua changamoto mpya ya kutokomeza njaa na hawana shaka kuwa atafikia lengo hilo.

Mourinho ambaye mkewe MAtile naye pia anateuliwa kuwa balozi maalum wa WFP kwa mpango wa utoaji vyakula shuleni, wiki ijayo atatembelea operesheni kadhaa za WFP zinazotekelezwa kwenye nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.

Akizungumzia uteuzi huo Mourinho amesema kuunga mkono operesheni za WFP za kutokomeza njaa ni uamuzi wake binafsi ambao yeye na familia yake wanaupenda.

Mourinho anaungana na watu wengine mashuhuri wenye nyadhifa hiyo ya kutokomeza njaa kama vile mwigizaji sinema Drew Barrymore, mwimbaji Cristina Aguilera na mcheza soka Ricardo Kaka.