Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaunda kamisheni kupatia suluhu utipwatipwa miongoni mwa watoto

Mkutano wa kikao cha 67 cha baraza kuu la WHO (Picha ya WHO/V. Martin)

WHO yaunda kamisheni kupatia suluhu utipwatipwa miongoni mwa watoto

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la afya duniani, WHO Dkt. Margaret Chan amesema ana wasiwasi mkubwa kutokana na kasi kubwa ya ongezeko la idadi ya watoto wenye unene kupita kiasi au utipwatipwa duniani katika nchi za vipato vya chini na kati hususan barani Afrika.

Amesema hayo wakati akiifungua kikao cha 67 cha baraza kuu la shirika hilo mjini Geneva…

(Sauti ya Dkt. Chan)

"Barani Afrika pekee, idadi ya watoto tipwatipwa imeongezeka kutoka Milioni Nne mwaka 1990 hadi Milioni 10 mwaka 2012. Hii inatia hofu. Kama ripoti ya takwimu ya afya mwaka 2014 inavyosema bayana.. Watoto wetu wanazidi kuwa wanene kupindukia. Ili kupata ushauri wa kushughulikia janga hili nimeunda kamisheni ya ngazi ya juu kumaliza utipwatipwa miongoni mwa watoto”

Dkt. Chan amesema ni bahati nzuri kwamba Sayansi inatoa fursa mbadala za kumaliza tatizo hilo na ni matumaini yake kamisheni hiyo itaibuka na ripoti ya aina yake yenye mapendekezo ambayo yatawasilishwa kwenye kikao cha baraza hilo mwakani.