Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO na EU waazimia kukarabati urithi wa kitamaduni wa Timbuktu

Nembo ya UNESCO

UNESCO na EU waazimia kukarabati urithi wa kitamaduni wa Timbuktu

Mkurugenzi wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO nchini Mali Lazare Eloundou Assomo na Kamishna wa Muungano wa Ulaya kuhusu Maendeleo, Andris Piebalgs, leo wamesaini makubaliano ya kufadhili ukarabati wa maeneo ya urithi wa kitamaduni ya Timbuktu, Mali.

Wakati wa hafla ya kutia saini makubaliano hayo, Kamishna wa Ulaya Andris Piebalgs amesema ukarabati wa urithi huo wa kitamaduni ambao Mali inajivunia, utachangia siyo tu maridhiano baina ya jamii, bali pia ukwamuaji wa uchumi kupitia utalii.

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Irina Bokova, amekaribisha usaidizi unaotolewa kwa Mali na Muungano wa nchi za Ulaya na wafadhili wengine, akisema kuwa makubaliano hayo ya leo yanaashiria kufuata mkondo upasao. Amesema makaburi mawili ya wafalme wa zamani wa Mali sasa yamejengwa, na kwamba hatua hiyo ya leo itaongeza kasi ya kukamilisha kazi ya ukarabati, ili watu wa Mali wajivunie tena urithi wao wa pamoja wa kitamaduni, ambao unaweza kuleta maridhiano.

Makaburi 14 kati ya 16 ya Timbuktu, ambayo yameorodheshwa na UNESCO kama Maeneo ya Urithi wa Dunia, yaliharibiwa na makundi yenye silaha wakati wa mgogoro nchini Mali. Daftari 4,000 za maandishi ya kihitoria kutoka karne ya 13 kati ya daftari 40,000 zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye Taasisi ya Ahmed Baba, pia zilipotoea.