Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutetea mashoga ni jambo sahihi na la haki : UM

Katibu Mkuu Ban Ki-Moon akiwa na ujumbe mahsusi kwa siki ya tarehe 17 Mei. (Picha-Umoja wa Mataifa)

Kutetea mashoga ni jambo sahihi na la haki : UM

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kupinga ubaguzi dhidi ya wapenzi wa jinsia moja, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amesema kundi hilo bado linapata ubaguzi kuanzia majumbani mwao hadi maofisini hata kama kuna sheria zinazowatetea.Katika ujumbe wake Ban amesema majumbani wanatelekezwa, shuleni wanaburuzwa na maofisini hunyanyapaliwa na hata kukataliwa kuajiriwa kisa tu mtu ni shoga, msagaji au amebadili jinsia yake, LGBT.

Ban amesema kila mtu ana haki ya kuishi vile anavyotaka na kumpenda mtu amtakaye. Hata hivyo amesema licha ya kwamba nchi zinapaswa kuchukua hatua zaidi kulinda haki za mashoga na wapenzi wa jinsia moja, amesifu nchi 62 ambazo sasa zina sheria zinazopinga ubaguzi kwa misingi ya jinsia ya mtu. Amesema ni sahihi kubadili sheria lakini kubwa zaidi ni kubadili mtazamo wa jamii dhidi ya kundi hilo.

Mtaalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kutoka shirika la mpango wa maendeleo, UNDP Clifton Cortez ameiambia Radio ya Umoja wa Mataifa kuwa utetezi wa kundi hilo ni jambo la hatari hususan katika maadhimisho kama ya siku hii lakini ni jambo vema na sahihi kulifanya.

(Sauti ya Cortez)

“Bila shaka kuna hatari, na ni jambo ambalo tunapaswa kujiandaa kuchukua hatua. Kila wakati tumeweza kuchukua hatua stahili kwa njia sahihi katika kila mazingira. Lakini nafananisha na matukio mengine ya harakati za haki za binadamu duniani kote katika historia ya dunia, kama miji ya New York, hapa nitazungumzia Marekani kwa dakika chache! Nni hatari hiyo hiyo ambayo Wamarekani wenye asili ya Afrika na washirika wao walichukua walipoanza maandamano kusaka haki za raia miaka ya 50 na 60. Tunajua bila shaka ilikuwa na mafanikio makubwa na lilikuwa ni jambo sahihi, na kwa hili halina tofauti.”