Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viwango vya matarajio ya uhai wa mwanadamu vimepanda: WHO

Mwanamume mzee akitunza mimea (Picha ya WHO / SEARO /Anuradha Sarup)

Viwango vya matarajio ya uhai wa mwanadamu vimepanda: WHO

Watu kote duniani sasa wanaishi kwa muda mrefu zaidi, kwa mujibu wa takwimu mpya za afya duniani ambazo zimetolewa na Shirika la Afya Duniani, WHO. Joshua Mmali na taarifa kamili

TAARIFA YA JOSHUA

Kulingana na takwimu za afya kwa mwaka 2014, WHO imesema, kutokana na viwango wastani vya kimataifa, msichana ambaye alizaliwa mwaka 2012 anaweza kutarajia kuishi hadi atimu umri wa miaka 73, huku mvulana aliyezaliwa mwaka huo akitarajia kuishi hadi umri wa miaka 68. WHO inasema hiyo ni miaka sita zaidi kuliko kiwango wastani cha matarajio ya uhai wa mtoto aliyezaliwa mwaka 1990.

Ripoti hiyo ya kila mwaka ya tawkimu za afya za WHO inaonyesha kuwa nchi za kipato cha chini zimepiga hatua kubwa zaidi, kwa kuongezeka viwango wastani vya uhai kwa miaka 9 kutoka mwaka 1990 hadi 2012.

Miongoni mwa nchi sita ambako viwango wastani vya matarajio ya uhai vimeongezeka zaidi ni Liberia, ambako kimeongezeka kutoka miaka 42 hadi 62, Ethiopia (45 hadi 65), Maldives (58 hadi 77), Cambodia (54 hadi 72), Timor Leste (50 hadi 66) na Rwanda ambako kimepanda kutoka miaka 48 hadi 65).

Ties Boerma ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Takwimu katika WHO anaeleza ni kwa nini hali imebadilika

SAUTI YA TIES BOERMA

Kwanza, malengo ya Milenia kuhusu afya yameleta ufanisi mkubwa na kuchangia kuboresha hali, hususan katika nchi za kipato cha chini. Vifo vya watoto vimepungua kwa asilimia 47 tangu 1990, vifo vya wajawazito, vimepungua kwa asilimia 45. HIV, TB, malaria- maambukizi mapya na vifo vimepungua.Lakini pia tukubali kuwa nchi nyingi hazitatimiza MDGs, kama ilivyo wazi katika ripoti hii”