Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Natumai Baraza kuu litashughulikia kwa kasi suala la Dag Hammarskjöld: Ban

Katibu Mkuu wa UM Ban Ki-Moon akiwa na Waziri Mkuu wa Sweden, Frederik Reinfeldt wakati wa mkutano na waandishi wa habari. (Picha:UM//Paulo Filgueiras)

Natumai Baraza kuu litashughulikia kwa kasi suala la Dag Hammarskjöld: Ban

Nimeliomba Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuongeza suala la uchunguzi wa kifo cha aliyekuwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Dag Hammarskjöld katika ajenda zake kutokana na ushahidi mpya uliojitokeza.

Ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari mjini Stockholm, Sweden aliko ziarani kikazi.

Mwandishi wa habari alitaka kufahamu kitakachofuatia baada ya ripoti mpya ambapo kuhusu kifo hicho kutolewa ambapo Ban amesema pamoja na kuwaomba waweke ajenda hiyo pia ametaka waangalie kwa mapana zaidi suala hilo la kifo cha Hammarskjöld kilichotokea mwaka 1961 kwa ajali akiwa anaelekea Congo-Kinshasa, kusaka suluhu la mzozo.

Amesema ametoa mapendekezo kadhaa kwa Baraza Kuu na anaamini ni vyema kufahamu kile hasa kilitokea juu ya kifo chake, na iwapo chanzo kilikuwa tatizo la kiufundi la ndege alimokuwa akisafiria, au mchezo mchafu au pengine jaribio la kumuua Katibu Mkuu huyo wa Pili wa Umoja wa Mataifa.

Bwana Ban amesema hilo ni suala nyeti na ni lazima kupata ukweli na ana mategemeo makubwa kwa kasi itakayochukuliwa na Baraza Kuu juu ya suala hilo.

Mkutano huo na waandishi wa habari ulihudhuriwa pia na Waziri mkuu wa Sweden Frederik Reinfeldt ambaye awali akiwa na Bwana Ban kwenye mazungumzo yao walijadili mizozo inayoendelea Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ukraine na hali ilivyo Cyprus. Ban ameshukuru Sweden kwa inavyojitoa kusaidia jitihada za Umoja wa Mataifa.