Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yakaribisha makubaliano ya amani huko Jonglei

UNMISS

UNMISS yakaribisha makubaliano ya amani huko Jonglei

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini, UNMISS umepongeza makubaliano ya tarehe Tisa mwezi huu ya kuleta amani ya kudumu kwenye eneo la Pibor jimbo la Jonglei.

Mwakilishi wa kudumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini na Mkuu wa UNMISS Hilde Johnson amesema makubaliano hayo kati ya serikali na kikundi kilichojihami cha South Sudan Democratic Movement al Maarufu Cobra yataleta utulivu kwenye eneo hilo ambalo miezi sita iliyopita kabla ya kuanza kwa mzozo wa sasa, lilikuwa kitovu cha ukosefu wa utulivu nchini humo.

Amesifu jopo la usuluhishi la kanisa lililowezesha kufikia kwa makubaliano hayo huko Addis Ababa, Ethiopia, halikadhalika pande husika kwenye mzozo huo akisema kuwa yataweka msingi wa amani ya kudumu kwa jamii zote za Pibor na maeneo yanayozunguka na UNMISS iko tayari kutoa usaidizi kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa.

Ametoa wito kwa wadau wa kimataifa na wasaidizi wa kibinadamu kusaidia serikali na wakazi wa eneo la Pibor kushughulikia chanzo cha ukosefu wa utulivu ikiwemo kuwapatia mahitaji muhimu na kuhakikisha wananchi wananufaika na makubaliano ya amani.

Bi. Johnson amesema ni matumaini yake kuwa serikali ya Sudan kusini na upinzani katika mzozo wa sasa unaoendelea watafuata nyayo za kilichotokea Pibor ili kumaliza mapigano yanayoleta machungu kwa wananchi.