Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni 33.3 ni wakimbizi wa ndani kote duniani: UNHCR/IDMC

kila dakika, familia moja inalazimishwa kuhama Syria. @UNHCR

Watu milioni 33.3 ni wakimbizi wa ndani kote duniani: UNHCR/IDMC

Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, likishirikiana na Kamati ya wakimbizi ya Norway, NRC, leo mjini Geneva zimetangaza ripoti yake kuhusu hali ya wakimbizi wa ndani mwaka 2013, takwimu zikionyesha idadi ya wakimbizi imefika kiwango cha kuvunja rekodi. Taarifa kamili na Priscilla Lecomte

Akizungumza leo mbele ya waandishi wa habari, pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, Jan Egeland, Katibu Mkuu wa NRC amesema idadi hii ya wakimbizi wa ndani imefika milioni 33.3, kiwango ambacho hakijawahi kufikishwa.

Ameongeza kueleza kwamba nchi tano tu zinachangia kwa asilimia 63% ya idadi ya wakimbizi, zikiwemo Syria, Colombia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan na Nigeria kwa mara ya kwanza, kwani serikali ya Nigeria imeandaa takwimu mpya.

Tofauti na wakimbizi wengine, amesema wakimbizi wa ndani…

“ Hawa watu wako kwenye hali ya mgogoro mbaya zaidi. Hawana usalama, hawapati misaada yeyote, hawa ndio wanaishi kwenye mazingira magumu kuliko wote wengine duniani”

Jan Egeland ameongeza, kasi hii ya ongezeko la wakimbizi wa ndani siyo kitu kinachokubalika kuendelea, akitoa wito kwa suluhu la kisiasa kwa mizozo na vita vya ndani.

“ Suluhu la kudumu ni nini? Ni maendeleo, ni harakati za amani, ni kulinda haki za walio wachache, ni suluhu la kisiasa na la kimaendeleo, lakini hivi sasa hayapatikani.”