Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maamuzi ya kisiasa ya AU hayawezi kuathiri uendeshaji mashataka ICC: Bensouda

Maamuzi ya kisiasa ya AU hayawezi kuathiri uendeshaji mashataka ICC: Bensouda

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, Fatou Bensouda, amesema kuwa maamuzi ya kisiasa yaliyofanywa na nchi wanachama wa Muungano wa Nchi za Afrika, AU, hayawezi kuathiri shughuli za uendeshaji mashtaka katika mahakama hiyo.

Bi Bensouda amesema hayo akijibu swali kuhusu uhusiano wa ICC na nchi za Afrika, katika mkutano na waandishi wa habari mjini New York, mara tu baada ya kulihutubia Baraza la Usalama kuhusu kesi za Said al Gaddafi na Abdella al Sanousi wa Libya.

Mwanasheria huyo wa kimataifa amesema Mahakama ya ICC imeendelea kuwasiliana na nchi za Afrika, hususan zile nchi binafsi zinazoshirikiana nayo, na kwamba wataendelea kuzungumza na nchi wanachama wa AU, ili zipate ufahamu zaidi kuhusu jinsi Mahakam hiyo inavyofanya kazi.

“Tutaendelea kuwasiliana na AU, kwani mjuavyo, idadi kubwa ya nchi zilizoridhia Mkataba wa Roma, zinatoka Afrika, kwa hiyo tutaendelea kuwasiliana nao. Hata tumepanga warsha ya mafunzo mwezi Julai kwenye ngazi ya kitaaluma, kati ya Afrika na AU, ili kuendeleza mazungumzo tuliyo nayo.”