Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Brahimi asikitika kuiacha Syria katika hali mbaya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na Lakhdar Brahimi (Picha ya UM/JC McIlwaine

Brahimi asikitika kuiacha Syria katika hali mbaya

Ni Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon katika utangulizi wa taarifa yake ya kutangaza kujiuzulu kwa Mjumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa nchi za kiarabu katika mzozo wa Syria, Lakhdar Brahimi. Ban anasema ni kwa masikitiko makubwa ya kwamba baada ya mashauriano na Nabil El Araby, Katibu Mkuu wa Muungano wa nchi za kiarabu ameamua kukubali kujiuzulu kwa Brahimi kuanzia tarehe 31 mwezi Mei mwaka huu.

Bwana Ban amesema kwa takribani miaka miwili Brahimi amejitahidi kumaliza machungu ya wananchi wa Syria, na kwa muda mrefu ametambuliwa kuwa mwanadiplomasia wa kipekee na mtetezi wa misingi  ya katiba ya Umoja wa Mataifa na hivyo suala la kuyeyuka kwa lengo lake la kutumia kipaji chahe kusuluhisha mzozo huo ni janga kwa Syria.

 Kwamba jitihada zake hazikupata uungwaji mkono wa kutosha kutoka chombo cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na amani na usalama na kutoka nchi zenye ushawishi na hali ya Syria, hii ni kushindwa kwetu sote.”

 Ban pia akageukia Syria..

“Nasikitika kuwa pande husuka hususan serikali zimekuwa zinasita kutumia fursa ya kumaliza janga la nchi hii. Narejelea wito wangu wa kutaka waonyeshe busara na uwajibikaji ambao utaruhusu kuondokana na jinamizi hili. Halikadhalika nasisitiza tena mtazamo wangu kuwa lazima kuwepo uwajibikaji kwa uhalifu uliofanyika na unaoendelea kutendeka ikiwemo jamii kuachwa na njaa kwa kuzuia misaada ya kibindamu kuwafikia.”

Fursa ikawadia kwa Bwana Brahimi ambaye hakuficha hisia zake kwa vile anavyoiachaSyria..

Ni jambo la kusikitisha kuwa naicha Syria katika hali mbaya. Lakini kama ulivyosema Katibu Mkuu, sina shaka kuwa utaendelea kama ambavyo umekuwa unafanya kuchukua kila hatua inayowezekana kushirikiana na Baraza la Usalama, majirani wa Syria na bila shaka pande husika za Syria zenyewe kumaliza mzozo huu.”

Kujiuzulu kwa Brahimi aliyeteuliwa kushika wadhifa huo mwezi Agosti mwaka 2012 kunakuja wakati huu ambapo mzozo huo umeingia mwaka wan nne huku zaidi ya watu Laki Moja wakiwa wamemeuawa na mamia ya maelfu kadhaa wamesaka hifadhi ndani na nje ya nchi yao.