Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kupiga vita umaskini ndio mwarobaini wa ujangili wa tembo na biashara haramu ya wanyamapori

Mkuu wa UNDP Helen Clark akizungumza na Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda. (Picha-UNDP)

Kupiga vita umaskini ndio mwarobaini wa ujangili wa tembo na biashara haramu ya wanyamapori

Msimamizi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo katika Umoja wa Mataifa, UNDP, Helen Clark, amehitimisha ziara yake nchini Tanzania ambako amekuwa akihudhuria kongamano lililowaleta pamoja wadau kutoka sekta mbali mbali nchini humo, kwa minajili ya kutafutia suluhu tatizo la ujangili wa tembo na biashara haramu ya wanyama wa pori. Grace Kaneiya na taarifa kamili

Bi Clark ambaye amekutana na waandishi wa habari mjini Dar Es Salaam mwishoni mwa ziara yake hiyo, amesema ameshuhudia utashi wa kutosha miongoni mwa wote walioshiriki kongamano hilo kufanya kila wawezalo kuchangia katika kukomesha uwindaji wanyama pori na ujangili wa tembo na ulanguzi wa bidhaa kama pembe. Bi Clark amesema ni kazi ngumu, lakini inawezekana

“Hatua nyingi ndogo kwenye mkondo ufaao zitachangia pakubwa katika kupiga vita ujangili na ulanguzi huu. Baadhi ya hatua hizo ni kuwapa mafunzo walinzi wa mbuga za wanyama, vifaa bora na kuzisaidia jamii za mashinani ili zifaidike kutokana na kuwalinda wanyama pori na siyo kuwaua”

Bi Clark pia amesema hatua muhimu zaidi kati ya zote hizo ni kupiga vita umaskini

“Suluhu kwa tatizo la ujangili linapatikana katika sehemu kadhaa. Kadri watu wanavyoendelea kuwa maskini, ndipo watu wanapopata shinikizo la kulipwa na majangili. Kwa hiyo kukabiliana na maendeleo ya vijijini na fursa za riziki zitakuwa hatua muhimu sana za kupiga vita uhalifu huu hapa na kwingineko”