Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban awataka Waisraeli na Wapalestina wachague suluhu la mataifa mawili

KM Ban Ki-moon

Ban awataka Waisraeli na Wapalestina wachague suluhu la mataifa mawili

Mkwamo wa sasa wa kisiasa kuhusu suala la harakati za amani kati ya Israel na Paletsina unahatarisha kwa kiasi kikubwa matumaini ya kuwepo kwa suluhu la mataifa mawili, na kuendelea kutochukua hatua kunaweza kuzorotesha utulivu zaidi. Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon, katika hotuba yake iliyosomwa na Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu harakati za amani Mashariki ya Kati, Robert Serry wakati wa kufungua mkutano wa kimataifa kuhusu suala la Jerusalem, mjini Ankara, Uturuki.

Mkutano huo unalenga kuimarisha uungwaji mkono wa kimataifa kwa utafutaji suluhu la kudumu kuhusu suala la Jerusalem.

Bwana Ban katika ujumbe huo amesema pande zote zinapaswa kutambua kuwa kutofanya uchaguzi unaopendelea amani na kuishi pamoja katika utaratibu wa mataifa mawili ndio uchaguzi mbaya zaidi. Ameongeza kuwa kutoendeleza mazungumzo ya kupata suluhu la mataifa mawili kutaendeleza hali ya kuwepo tu taifa moja, na hivyo kutoa wito kwa pande zote kujiepusha na hatua za kibinafsi ambazo zitachangia kutatanisha hali zaidi na kudhoofisha matumaini ya kurudia meza ya mazungumzo.

Ban amesema ujenzi wa makazi kwenye Ukingo wa Magharibi na Mashariki mwa Jerusalem ni kinyume na sheria ya kimataifa, na ni kikwazo kikubwa katika kutafuta amani, akiongeza kuwa kubomoa nyumba za Wapalestina na uharibifu wa mali zao ni kinyume na wajibu wa Israel wa kuwalinda raia walio chini ya mamlaka yake.