Ban ateua mwanamke wa kwanza kuongoza kikosi cha kulinda amani cha UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon na Meja-Jenerali Kristin Lund (picha ya UM/Mark Garten)

Ban ateua mwanamke wa kwanza kuongoza kikosi cha kulinda amani cha UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameendelea kutekeleza azma yake ya kuongoza kwa vitendo katika suala la usawa wa kijinsia kwa kumteua Meja-Jenerali Kristin Lund wa Norway kuwa Kamanda wa kwanza mwanamke wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa.

Taarifa ya Msemaji wa Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa Meja Jenerali Lund ataongoza kikosi cha kulinda amani cha wa Umoja wa Mataifa nchini Cyprus, UNFICYP baada ya Meja Jenerali Chao Liu wa China kumaliza muda wake tarehe 13 Agosti mwaka huu.

Bwana Ban kupitia taarifa hiyo ameshukuru mchango wa Meja Jenerali Liu katika jitihada za amani za Umoja wa Mataifa huko Cyprus huku akisema kuwa Meja Jenerali Lund ana weledi katika nyanja ya kijeshi kwa zaidi ya miaka 34 ikiwemo uongozi wa kijeshi katika ngazi za kitaifa na kimataifa.

Mathalani huduma yake katika kikosi cha muda cha Umoja wa Mataifa Lebanon, UNFIL na kuanzia mwaka 2007 hadi 2009 alikuwa Naibu Kanada wa majeshi ya Ulinzi nchini Norway.

Meja Jenerali Lund ana shahada ya uzamili katika masuala ya mikakati kutoka Chuo cha masuala ya kijeshi nchini Marekani.