Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano kuhusu masuala ya watu wa asili laanza mjini New York

Kongamano kuhusu masuala ya watu wa asili laanza mjini New York

Zaidi ya watu wa asili 1500 wanatarijiwa kuhudhuria kikao cha kudumu cha Umoja wa Mataifa kinachojadili masuala ya makabila asili kinachoanza leo mjini New York. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

(Taarifa Priscilla)

“Utawala Bora unamaanisha kuheshimu na kutunza haki za watu wa asili”, amesema Dalee Sambo Dorough, Mwenyekiti wa kikao hicho, akieleza kuwa kikao cha mwaka huu kitamulika hali ya watu wa asili wanaoishi barani Asia, ambao wanakabiliana zaidi na ubaguzi wa kiuchumi, kijamii, na kisiasa, wakati ni sehemu wanapoishi zaidi ya asilimia 60 ya watu wa asili duniani. Katika mazungumzo ya wiki hii, washiriki watazingatia umuhimu wa kutambua lugha na tamaduni za asili, na kupigania haki zao za kujitegema.

Changamoto nyingine kubwa ni pamoja na umiliki wa ardhi na matumizi ya rasilimali, wakati utandawazi na ukuaji wa uchumi vinaweka shinikizo kubwa juu ya ardhi za watu wa asili.

Wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amezungumzia pia mchango wa watu wa asili:

“Mahitaji, Sauti na Michango ya watu wa asili ni sehemu kubwa ya kutimiza maendeleo endevu baada ya mwaka 2015, hasa kwa upande wa mabadiliko ya tabianchi. Ujuuzi wao wa asili na tabia zao zinaweza kusaidia katika kupunguza utoaji wa gesi chafuzi na kuelekea katika maendeleo endelevu zaidi.Nawaomba nchi wanachama kutambua umuhimu wa watu wa asili katika changamoto ya mabadiliko ya tabianchi”