Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waathiriwa wa ukatili wa kingono DRC wanahitaji haki: Bangura

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kingono katika vita, Zainab Hawa Bangura(Picha ya UM)

Waathiriwa wa ukatili wa kingono DRC wanahitaji haki: Bangura

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kingono katika vita, Zainab Hawa Bangura, ameelezea kukatishwa tamaa na uamuzi uliofanywa na mahakama dhidi ya washukiwa wa vitendo vya ubakaji wa Mionova katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, ambapo ni watu wawili tu waliopatikana na hatia ya kosa la ubakaji.

Bi Bangura amesema amesikitishwa na hukumu hiyo, akisema uamuzi huo haulingani na ukubwa wa uhalifu wa ukatili wa kingono uliofanywa, na kwamba umeshindwa kuwapa haki waathiriwa waote ambao walikuwa na ujasiri wa kupeleka kesi hiyo kotini.

Amewapa heko manusura wa ukatili huo kwa ujasiri wao, na kutoa wito kwa mamlaka za DRC kuwalipa fidia na kuchukua hatua mara moja za kuwalinda manusura, mashahidi na mawakili waliofanya bidii kutafuta haki kwa mamia ya manusura, pamoja na watetezi wa haki za binadamu waliopigania uwajibikaji.