Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakulima Ufilipino wapata mavuno ya kwanza baada ya kimbunga:FAO

Mmoja wa wakulima ambao wameanza kuvuna mpunga huko Ufilipino baada ya kimbunga Haiyan. (Picha:Tovuti ya FAO)

Wakulima Ufilipino wapata mavuno ya kwanza baada ya kimbunga:FAO

Miezi sita baada ya kimbunga Haiyan kupiga Ufilipino na kusababissha madhara makubwa ikiwemo kupoteza maisha ya watu na mali, wakulima nchini humo hatimaye wamepata mavuno ya kwanza ya mpunga.

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema makumi ya maelfu ya wakulima sasa wanavuna mpunga wao baada ya kimbunga Haiyan kuhatarisha uhai na kipato chao kwani kilivuruga mashamba yao na hata shughuli za kilimo hazikuweza kufanyika.

Mavuno haya ya kwanza yanafuatia hatua za FAO na wadau wake ikiwemo serikali ya Ufilipino na jamii ya kimataifa ya kuwezesha wakulima kurejesha mashamba yao katika hali ya kawaida na kufanya shughuli za upanzi wakati msimu ulipowadia.

Rajendra Aryal ni mratibu mwandamizi wa opereshani za dharura FAO mjini Manila, Ufilipino anaelezea mavuno hayo.

 (Sauti ya Rajendra)

 “Kutokana na taarifa za awali tulizopokea wakulima wanahifadhi mavuno kwa matumizi yao na pia mbegu kwa ajili ya msimu ujao wa upanzi, halikadhalika kiasi kidogo cha mchele kinauzwa sokoni. Tumekutana na familia ambazo zimeweza kununua kuku na nguruwe kutokana na kipato kilichotokana na mauzo ya ziada ya mavuno.”

Kimbunga Haiyan kilipiga eneo la Kati la Ufilipino tarehe 08 Novemba mwaka 2013 na kusababisha vifo vya watu 6,000 huku ekari 600,000 za kilimo zikiharibiwa.