Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhaba wa mafuta CAR walazimu WFP kusafirisha shehena ya mafuta ya ndege kutoka Kenya

Lishe ya mtoto huyu iko mashakani Jamhuri ya Afrika ya Kati kutokana na ukosefu wa uhakika wa chakula bora. (Picha:WFP/Rein Skullerud )

Uhaba wa mafuta CAR walazimu WFP kusafirisha shehena ya mafuta ya ndege kutoka Kenya

Shirika la mpango wa chakula duniani, WFP limesema shehena ya mafuta ya ndege imesafirishwa kutoka Nairobi Kenya kuelekea mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bangui ili kuendeleza jukumu la kusambaza misaada ya ya chakula kwa wahitaji kutokana na mzozo unaoendelea nchini humo.

WFP imesema imeamua kuchukua hatua hiyo kutokana na uhaba wa mafuta nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati uliosababishwa na malori yenye shehena hiyo kushindwa kuvuka mpaka wa Camerooon kwa sababu ya ukosefu wa usalama.

Shehena ya tani Elfu 50 za mafuta aina ya Jet A-1 yenye thamani ya dola 280,000 inatarajiwa kusaidia usambazaji wa misaada kwa njia ya anga kwa takribani wiki tatu.

Mkurugenzi wa WFP kanda ya Afrika Magharibi Denise Brown amesema ni matarajio yake kuwa makubaliano yatafikiwa baina ya madereva, kampuni za mafuta, serikali na pande zote husika kwenye mzozo huo ili usafirishaji wa mafuta kwa njia ya barabara uweze kurejea mara moja na kuondoa uhaba wa sasa wa nishati hiyo adhimu.

WFP imesema hatua ya kusafirisha shehena hiyo ya mafuta kwa njia ya ndege itakuwa na gharama kubwa lakini haina njia nyingine kwa kuzingatia wajibu wake wa kusambaza msaada wa vyakula kwa wahitaji ikiwemo watoto 25,000 wanaokabiliwa na utapiamlo uliokithiri.

Theluthi mbili za wanaopokea msaada wa chakula kutoka WFP wanaishi vijijini nje ya mji mkuu Bangui kwenye maeneo ya Bambari, Bossangoa, Bouar, Kaga Bandoro na Paoua.