Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutokomeza njaa kunawezekana: Ban

Kutokomeza njaa kunawezekana: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, amesema leo kuwa ni vigumu kufikia malengo ya kutokomeza umaskini uliokithiri na maendeleo endelevu bila kutokomeza njaa. Taarifa ya Joshua Mmali ina maelezo zaidi.

JOSHUA TAARIFA

Katibu Mkuu amesema lengo la kutokomeza njaa linaweza kufikiwa, wakati akiihutubia Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu Usalama wa Chakula Duniani, ambayo inakutana mjini Roma, Italia. Ban amesema kamati hiyo inajitahidi kuhakikisha watu wana usalama wa chakula na lishe, kupitia mifumo endelevu ya kilimo, na kutaja kazi ya kamati hiyo kuwa muhimu sana duniani.

Katibu Mkuu ameongeza kuwa changamoto ya kutokomeza njaa, kuhakikisha uwepo wa chakula na kuifanya mifumo ya kilimo na chakula kuwa endelevu inahitaji mikakati ya pamoja, na kusema kuwa itahitaji pia kuongeza kasi ya juhudi za kufikia lengo la maendeleo (MDG) kuhusu njaa, wakati ukomo wa malengo ya milenia ukikaribia.

“Hatuwezi kutokomeza umaskini uliokithiri au kufikia maendeleo endelevu bila kuwa na chakula na lishe ya kutosha kwa watu wote. Hatuwezi kupata amani au usalama ikiwa mtu mmoja kati ya wanane ana njaa. Hatuwezi kusema kuwa tumefikia malengo yetu hadi pale kila mwanamume, kila mwanamke na kila mtoto atakapopata haki ya kuwa na chakula cha kutosha.”

Ban amesema suala la usalama wa chakula linatakiwa liwekwe kwenye ajenda ya maendeleo baada ya 2015, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia pia mabadiliko ya tabinanchi na haja ya kuwasaidia wakulima kuwa na uhimili wa mabadiliko hayo.