Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisi ya haki za binadamu yasikitishwa na hukumu za wahalifu wa ukatili wa kingono Minova, DRC

Ofisi ya haki za binadamu yasikitishwa na hukumu za wahalifu wa ukatili wa kingono Minova, DRC

Ofisi ya Haki za Binadamu, OHCHR, imekiri leo kusikitishwa na hukumu zilizotolewa na mahakama ya kijeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC kuhusu kesi za ukatili wa kingono huko Minova.

Mwezi Novemba mwaka 2012, ripoti za Umoja wa Mataifa zilituhumu askari wa jeshi la serikali FADRC, kutenda ukatili wa kingono ikiwemo kubaka idadi kubwa ya wanawake katika kijiji cha Minova, maeneo ya Goma, baada ya kushindwa mapigano dhidi ya waasi wa M-23.

OHCHR imesema kwamba, kati ya askari 39 walioshtakiwa na kesi 135 za ubakaji, ni askari wawili tu wamehukumiwa kwa ubakaji na mmoja na mauaji huku waliobakia wakiruhusiwa au kuhukumiwa na kesi za wizi tu.

Rupert Colville, ambaye ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu, amesema hawajaridhishwa na maamuzi hayo, akiongeza kwamba hakuna uwezekano wa kukata rufaa, na sheria hii ni dhidi ya katiba ya DRC na vilevile dhidi ya sheria ya kimataifa.

Sauti ya Colville

“ Uhalifu uliotokezea Minova na maeneo yake, mwezi Novemba, mwaka 2012 ulikuwa wa kiwango kikubwa na kibaya mno. Kwa mujibu wa ripoti ya umoja wa mataifa iliyotolewa baada ya uhalifu huo, zaidi ya vitendo 135 vya ukatili wa kingono vilitekelezwa na askari wa FADRC. Kwa hiyo inasumbua sana kuona kwamba hukumu mbili tu za ukatili wa kingono zilichukuliwa, wakati vitendo vya ukatili wa kingono vilikuwa vingi sana.”

Ripoti ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO pamoja na OHCHR iliyotolewa mwezi uliopita kuhusu mafanikio na changamoto katika kutokomeza ukwepaji wa sheria wa ukatili wa kingono nchini humo ilionyesha kwamba bado kuna hali ya ukwepaji wa sheria nchini humo.

Wakati ule, mkuu wa OHCHR, Navy Pillay, alitoa wito kwa serikali ya DRC itekeleze uchunguzi unaofaa kwa haraka na njia huru, ishtaki wanaoshukiwa, wakiwemo wanaojibika kwa ngazi za juu.