Hukumu dhidi ya Germain Katanga kutolewa 23 Mei: ICC
Mahakama ya kimataifa ya uhalifu, ICC huko The Hague, Uholanzi leo imetangaza tarehe 23 mwezi huu wa Mei kuwa siku ya kutoa hukumu dhidi ya Germain Katanga.
Katanga alipatikana na hatia katika makosa matano kati ya Kumi ikiwemo uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.
Uamuzi wa leo umetokana na kikao cha wazi cha jana na leo baada ya pande husika kwenye kesi hiyo kuwasilisha taarifa zao kuhusu hukumu stahili dhidi ya Katanga.
Nyaraka za kisheria za ICC zinaeleza kuwa majaji wanaweza kumpatia hukumu ya kifungo pamoj ana faini au kunyan’ganya mali zilizopatikana kwa uhusiano wa moja kwa moja au la na uhalifu aliofanya.
Halikadhalika zinasema kifungo hakiwezi kuzidi miaka 30 labda ithibitike kuwa uhalifu aliotenda ulikuwa na madhara makubwa ambapo anaweza kupatiwa kifungo cha maisha.
Hata hivyo idadi ya miaka ambayo mshtakiwa ameshakuwepo rumande itapunguzwa katika hukumu atakayopatiwa na majaji.
Kesi ya Katanga anayedaiwa kuwa kamanda wa kikosi cha FPRI huko Ituri Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ilianza kusikilizwa tarehe 24 Novemba mwaka 2009.