Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wachukua uongozi kuelimisha wenzao ili kuepuka ujinga: UNHCR

Walimu wakimbizi wanawafundisha waSudan Kusini watoto (Picha ya UNCHR)

Wakimbizi wachukua uongozi kuelimisha wenzao ili kuepuka ujinga: UNHCR

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesema pamoja na ukoaji maisha kuwa kipaumbele kwa wakimbizi wa Sudan Kusini nchini Ethiopia, suala la elimu kwa watoto wao linasalia kuwa kipaumbele kikubwa. Ripoti ya Grace Kaneiya inafafanua zaidi.

(Taarifa ya Grace)

Katika kambi kubwa zaidi ya wakimbizi wa Sudan Kusini nchini Ethiopia, Leitchuor elimu kwa wakimbizi inatolewa na wakimbizi wenyewe wakieleza kuwa hawataki watoto wao waendelee kuwa wajinga wa kutokujua kusoma na kuandika.

Elimu ni ya darasa la kwanza hadi la nne na walimu ni 17 wakitoka miongoni mwa wakimbizi 45, 000 kwenye kambi hiyo.

Mkuu wa shule hiyo Pal Wiw kutoka jimbo la Upper Nile anasema jukumu lao ni kutumia uzoefu wao kuelimisha ndugu zao, huku akitaka wanafunzi kuzingatia masomo kwa umakini.

Mratibu wa operesheni za dharura za UNHCR huko Gambella Alexander Kishara anasema awamu ya sasa ni bado ya dharura lakini wanasaka eneo zuri la shule na pindi wakipata watajenga shule nyingi zaidi.

Amesema wanatambua kuwa ni muhimu watoto warejee katika mfumo sahihi wa shule ili kusaidia kizazi kijacho cha Sudan Kusini.