Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu 750 waliuawa Iraq Aprili 2014 pekee

Nickolay Mladenov akiwahutubia waaandishi wa habari (Picha ya UNAMI)

Watu 750 waliuawa Iraq Aprili 2014 pekee

Jumla ya watu 750 waliuawa nchini Iraq na wengine 1,541 kujeruhiwa katika vitendo vya kigaidi na ghasia mwezi Aprili pekee, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa leo na Umoja wa Mataifa. Takwimu hizo hazijumuishi zile za watu waliouawa katika mkoa wa Anbar, ambako machafuko yamekuwa yakiendelea.

Kutoka vikosi vya usalama, idadi ya watu waliouawa ni 140, na waliojeruhiwa ni 230.

Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu Iraq ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNAMI, Nickolay Mladenov, amesisitiza haja ya kuwa na umoja na mbinu za kina katika kukabiliana na tishio la ugaidi nchini Iraq, wakati machafuko yanapoendelea. Ameongeza kuwa ni kupitia tu katika operesheni yakinifu za kiusalama, mazungumzo ya kisiasa na sera jumuishi za kijamii ndipo amani itaendelezwa.