Idhaa ya Kiswahili imeendelea kupanua wigo wake kimataifa

30 Aprili 2014

Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kamati ya habari ya Baraza Kuu la Umoja huo imeweka bayana vile ambavyo Idhaa ya Kiswahili imeendeleea kupanua wigo wake barani Afrika na ulimwenguni kwa jumla. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Ripoti ya Assumpta)

Idhaa ya Kiswahili ni miongoni mwa idhaa nane zinazorusha matangazo kuhusu habari za Umoja wa Mataifa na nchi wanachama ambapo Mkuu wa mawasiliano ya Umma kwenye Umoja huo Peter Launsky-Tieffenthal alisema idhaa hiyo imeongeza washirika wapya wa Radio na blogu za kijamii na kwamba wanatambua umuhimu wa Radio kwani bado ni tegemeo zaidi barani Afrika.

Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Ramadhani Muombwa Mwinyi akihutubia kikao hicho akapongeza hatua za Idara hiyo kuimarisha Idhaa ya Kiswahili lakini akasisitiza umuhimu wa Radio licha ya kuwepo kwa matangazo kupitia intaneti.

(Sauti Balozi)

“Wakati tunapendekeza matumizi ya teknolojia za kisasa za mawasiliano, bado tunaamini radio itabakia kwa miaka mingi ijayo kama njia muhimu zaidi ya kuhabarisha kwa nchi zinazoendelea hususan maeneo ya vijijini. Kwa mantiki hii ujumbe wangu unatambua kuwa idhaa za Kireno na Kiswahili zilizopatiwa watendaji kamilifu zimepata washirika wapya. Mfano idhaa ya Kiswahili imeongeza washirika wapya siyo tu Maziwa makuu bali pia Marekani.”

Hivi sasa matangazo ya Idhaa ya Kiswahili licha ya kupatikana kupitia tovuti yake radio.un.org/sw, mitandao ya kijamii na Radio washirika zilizoko Afrika na Marekani, pia yaweza kusikiliza billa gharama kwa wakazi wa Marekani na Afrika Kusini, na mipango ya kupanua wigo inaendelea.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter